Tuesday 13 February 2018

WEMA WA KUOZA?


Siku nenda siku rudi, tunashuhudia sakata ya makali ya kiangazi na njaa nchini pasi na matumaini ya kupata suluhisho la kudumu. Vyombo vya habari hutupa taswira ya kutamausha kwa kuangazia swala nyeti la kiangazi na baa la njaa.  Ni utu au uhayawani, tunapowakodolea macho kodo waathiriwa wa njaa huku tukila na kusaza? 
Image result for baa la njaa africa   
Image result for baa la njaa africaMaeneo ya Wajir, Baringo, Kilifi na maeneo mengine mbalimbali katika mkoa wa Kaskazini na Kaskazini Mashariki ni baadhi ya maeneo ambayo yameadhirika pakubwa kutokana na uhaba wa chakula. Wakaazi wa maeneo haya hukodolea kifo macho kwa kukosa hitaji la msingi mno (chakula). Je, maskini hawa wa Mungu wako katika dunia nyingine au hii moja wanaoishi mabwenyenye? Ahadi ya serikali ya kuwapa tumaini la kuishi walala hoi hawa litatimia lini?

Wana nyuso za kusikitisha, miili yao iliyokonda na kukondeana pia ni ya kughadhabisha, lakini nani wa kuwasaidia? Lisilobudi hubidi, na wao hawana budi ila kuamka kila uchao na kupambana na hali yao huku wakiwa na matumaini ya kupata afueni katika siku za usoni au kupitia kwa wasamaria wema. Huenda siku moja Maulana atafanya miujizi na masaibu wanayopitia waja hawa  yatatokomea milele, kwani serikali inayopaswa kuwajali, haijali togo wala jando. Ni wengi wamepoteza maisha yao, na kuwa kitoweo cha mauti, kwa ukosefu wa chakula. La haula!, sheria ya maskini haiko katika serikali ya mwenye navyo.

Mashirika yasiyo ya kiserikali alimaarufu (NGO's) kwa lugha ya kimombo, yamekuwa katika mstari wa mbele kwa kusaidia mikasa kama hii. Mashirika haya ambayo sana sana huwategemea wasamaria wema ili kutoa misaada yao, hujizatiti mno kwa kutoa huduma zao. Juhudi ambazo iwapo serikali ingeweza kuiga, basi majanga kama haya yangekuwa nadra sana. Cha kusikitisha ni kuwa, serikali ina uwezo mkubwa wa kuwasaidi maskini hohehahe hapa nchini, zaidi ya mashirika haya ya kibinafsi, ila ubinafsi na ufisadi uongozini, umesababishia kuwasahau wahusika wakuu wanaohitaji fedha za serikali.

Kila mwaka, bajeti inapotolewa, pesa hutengwa kwa mikakati ya sekta mbalimbali serikalini. Pesa hizi ni pamoja na pesa za kusaidia kukabiliana na majanga kama haya ya njaa na ukame nchini. Swali ni je, pesa hizi hutimiza kazi zilizokusudiwa au huishia mifukoni mwa watu binafsi?

Viongozi wetu wanapotoa misaada kwa majanga kama haya, wao huyafanya yaoneka kana kwamba ni jambo la kustaajabisha au kuvuliwa kofia. Wengi hujipigia debe na kujipiga kifua ili waonekane wachapa kazi, lakini ukweli ni kuwa, sivyo tudhaniavyo sisi. Katika asilimia mia ya pesa wanazopewa kuwasaidia watu mashinani, aslimia zaidi huishia katika mifuko yao. Kiwango cha msaada wanaotoa ni kidogo ghaya, na wakati wanapotoa wao huandamana na wanahabari na kujaza picha mitandaoni ili kuanikia wakenye jinsi walivyo wachapa kazi, ukweli ukiwa ni kinyume. Msaada wa hakika hauhitaji matangazo, sio lazima ugonge vichwa vya habari ndio uonekane kama msaada, kumbuka zuri chajiuza, kibaya chajitembeza.

Waswahili walinena kuwa, tenda wema nenda zako, wakaja wakaongeza kuwa, wema hauozi, lakini wema wa serikali yetu pamoja na uongozi wake ni wema wa aina gani? Ni wema huu, au uozo na unyama? Mtu mwenye akili timamu na mwenye utu ya binadamu anaweza kuwakodolea macho watu wanaokufa kutokana na njaa, ilhali pesa zinazostahili kuwasaidia, anajilimbikizia na kujiendelezea utajiri? Si huu ndio uhayawani aliyoimba msanii Nyashinski? Si haki kabisa!

    Image result for makali ya kiangazi afrika



2 comments:

  1. Ukweli mtupu, serikali should put in some extra effort... Nimeshindwa kucomment in pure swahili 😂😂

    ReplyDelete

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...