Monday, 25 September 2017

MOYO WANGU NAKUPA KAMA ZAWADI

"Sabrina! Sabrina! Fungua tafadhali! Mwanangu fungua tuyazungumzie." Babangu anayakatisha mawazo yangu huku akiubisha mlango kwa fujo na kujaribu kuufunga. "La baba, siwezi! Sitaki! Naomba uniache. Sitaki kumwona mtu yeyote kwa sasa." Nanyanyuka kitandani na kuelekea katika roshani ya chumba changu kilicho katika orofa ya nne. Moyo wangu unapiga kwa kasi huku nikiwa na hisia za kujirusha toka pale ghorofani na kujitoa uhai ili kutia kikomo machungu ninayoyapitia. Mawazo yanazidi kunikera na kunikereketa maini, hasa nikilitazama gauni langu nililovua na kutupa pale sakafuni. "Hivi Aly yuko wapi? Kuna uwezekano kuwa katekwa nyara? " Maswali hayaishi akilini. Nachukuwa simu yangu kutizama kama ametuma angalau hata ujumbe kunieleza aliko. La hasha! Sina ujumbe wowote, tena la kunitonesha kidonda zaidi ni kuwa simu yake ni mteja. Hivi ni nani kanipokonya tonge langu mdomoni?

Siku ilianza kwa furaha tele, furaha iliyozidi ya tasa aliyejaliwa mwana, leo ni siku iliyotarajiwa kuwa swadakta! Tulirauka che mbichi hata kabla ya jimbi wa kwanza kuwika. Pilka pilka za hapa na pale zilizidi huku simu zikipigwa kila pembe ili kuhakisha kuwa kila kitu kinaenda sambamba jinsi ilivyotarajiwa. Mimi na wasimamizi wangu tulikuwa katika hoteli moja maarafu jijini. Mila na tamaduni zinamkashifu mume kumwona mkewe kabla ya harusi na hivyo  tulizitia maanani. Hata ingawa nilikuwa na furaha ajabu, moyoni nilijawa na uoga huku nikiomba siku yangu iwe ya kufana, wanavyotarajia bi harusi wengi. Ndoto yangu ilikuwa imetimia kwani siku iliyokuwa imesubiriwa kwa hamu na ghamu bila shaka ilikuwa imewadia. Siku yangu ya kuipa kisogo maisha ya uwana wali na kuwa mke wa mtu. Mke wa Aly, mume niliyempenda na kumwenzi kwa sana, kwa dhiki na faraja, kwa hali na mali, kwake nilifika.

Hakuna zuri likosalo dosari na kila adinasi ana udhaifu wake. Kipenzi niliyemchagua hakuwa tofauti na binadamu yeyote yule, ila sijui ni kwa nini babangu mzazi hakumpenda. Babangu ni moja wapo wa wanabiashara mashuhuri nchini na kwa hivyo ni wazi kama mchana kuwa ana utajiri mkubwa. Sina ubainifu wa hakika ni kwa nini hakumpenda Aly, ila kupitia kwa mazungumzo ya mara kwa mara, nadhani alimwona mwenye kitengo cha chini. "Ulimpendea nini lakini? Hivi huyu ataweza kukutunza jinsi ninayokutunza mimi babako?" Aliuliza mara nyingi, kila tulipomzungumzia Aly. Alijaribu kunishawishi kuvunja mahusiano yetu ila juhudi zake ziligonga mwamba.

"Harusi tunayo hatuna?" Sauti zilisikika hewani pindi tu nilipofikishwa kanisani. Shangwe na nderemo zilijaa huku viuno vikinenguliwa. Kanisa ilifurika watu wengi ajabu kupita kiasi cha matarajio yangu. Uoga ulinizidi huku moyo ukinidunda. Babangu alikuja kunilaki, "umependeza mwanangu!" Aliniambia.
Mandhari ya kanisani yalipendeza kutokana na maridadi ya vibofu na maua ya rangi ya manjano na nyeupe, ama kwa hakika palipambwa pakapambika. Rangi hizo ziliwiana na nguo walizovaa wasimamizi wangu, nami nilemetameta ndani ya gauni langu jeupe kama theluji.


Tulitarajia kumpata bwana harusi na wasimamizi wake wawe wamewasili pale kanisani lakini mambo yakawa kinyume, hivyo tukalazimika kuwasubiri.Muda ulizidi kuyoyoma nami nikajawa na wasiwasi. Minong'ono ilikolea huku hali ya sintofahamu ikishuhudiwa. Msimamizi wangu alilazimika kupiga simu ili kubaini ni kipi kilichojiri na hata kabla ya kubonyeza "ok" gari lao liliwadia, "waaahh...angalau" nilishusha pumzi.

Nilipigwa na butwaa wasimamizi waliposhuka na kueleza kuwa hawajui Aly aliko. "Aliji.execuze kwenda ku.recieve call flani, na ndio hakurudi." Alisema mmoja wa wasimamizi wake. "Atiii??!!" Sikuyaamini masikio yangu. Sielewi nilivyovua viatu na kuchomoka mbio kutoka pale kanisani, wala sijui hisia na matukio yaliyofwatia. Kioja cha kusikitisha. Sijui Mambo yalivyokwenda ila nilijikuta chumbani kwangu.

Usaliti ulioje? Mbona leo? Ni heri angeniambia mapema. Nashindwa kuelewa kiini cha Aly kuniacha kwenye mataa. Mbona kanipofua? Je, babangu anaweza kuwa mhusika? Sidhani kwani hata ingawa hakumpenda Aly, aligharamika kwa sana kuifanikisha siku ya leo. Nashindwa kuelewa kabisa, ama kwa hakika, jambo usilolijua ni usiku wa kiza.

 Nilimpenda sana Aly na kwa sasa sihisi kama ntapenda tena. Nilijitolea kimwili, kiakili na kivyovyote vile kuwa naye, ila ni kama sikupangiwa, mipango ya Mtrehemezi hakuna anayeweza kupangua. Labda nitajikaza ili niishi kwa taswira ya muda tuliyokuwa nao, maana kwa sasa najihisi mpweke. Nitabaki na machungu na vidonda vya mapenzi kwani kokote aliko Aly, moyo wangu ameunyofua.

3 comments:

  1. Waaaah na umetuwacha kwa mataa kama Aly. Hebu tuletee story yote, I was glued to the end

    ReplyDelete
  2. This comment has been removed by the author.

    ReplyDelete
    Replies
    1. Hahaaaaa, it is called suspense Mami,..Keep guessing 😊😊

      Delete

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...