Wednesday 27 September 2017

SIKUKUSUDIA ILA KWA SASA NI MAREHEMU.

Katika huzuni twaomboleza, katika huruma tumefarijiwa sisi tuliyofiwa. Tuko makuburini ambapo kanisa, ndugu na jamaa wameungana nasi ili kumpa mkono wa buriani mamangu. Namshukuru Mungu kwa kumpumzisha kwani aliteseka sana nyakati zake za mwisho. Aliugua saratani kwa muda mrefu na kuugua kwake kuliniathiri pakubwa. Hata ingawa namshukuru Mungu kwa kumpumzisha, binafsi nimebaki na upweke. Nilimzoea sana na ndiye aliyekuwa rafiki wangu wa karibu. Natafakari maisha yatakavyokuwa bila yeye na wazo la babangu linanipa kichaa! "Hivi Mungu mbona ukamsahau na huyu mzee?" Najiuliza! Mazishi yalikamilika vizuri, watu wakatawanyika nami nikarejea nyumbani.

Ni wakati wa jioni nami sina hamu ya kufanya chochote kile. Naelekea katika chumba changu cha kulala ili angalau nipumzishe akili. Kifo cha mamangu kilikuwa pigo kubwa kwangu Ila kwa upande mwingine ulinipa fursa ya kujitaftia uhuru. Uhuru ambao sharti ningeupigania, ili kujinasua kutoka kwenye minyororo ya utumwa. Ni mengi nimeyapitia mikononi mwa babangu mzazi, na kila nikiwaza machozi hunitiririka.

Babangu ni mmoja wa waumini tajika kijijini, tena mwenye sifa kemkem. Anapendwa na wengi na ni wa kuheshimika, ila kwangu mimi, ni mbweha aliyevalia ngozi ya kondoo au nimuite ibilisi mtu. Babangu alinidhalilisha na kunigeuza kijakazi, si wa kazi za nyumbani bali wa kumtimizia haja zake za kimapenzi. Alimtishia mamangu na kumlazimisha kunishawishi ili nikubali matakwa yake, kwani mamangu hakuwa na uwezo wa kumtosheleza kutokana na hali yake ya kiafya. " Mwanangu hatuna la ziada, tena katika hali yangu tutaishi vipi bila babako? Naomba umtimizie iwapo unanipenda na unataka uzidi kuniona hai. Naelewa uzito wa jambo hili ila itakuwa siri" Alinisihi mamangu.

Nilimchukia babangu, "hivi huyu ni babangu mzazi kweli?" Nilishindwa kuelewa. Mbona asingetafta mke mwingine? Au ndio kuikuza heshima yake na kuoneka mungwana? Maisha yalikuwa magumu, kumwona mamangu akiteseka na ugonjwa huku babangu akinilawiti kila uchao, bora nife! Nilishindwa kujidhibiti huku maisha yangu ikikosa mwelekeo. Niliathirika pakubwa hasa kisaikolojia, adhabu ilioje!

Usingizi ulinijia na kwa ghafla nikashtushwa na sauti ya babangu. "Mbona mapema leo mwanangu?" Sauti yake yenye uzito iliniamsha. Ni vipi nilisahau kuubana mlango? Sikuwa tayari kabisa kuzidi kumhudumia. Tena mamangu ndio kafa, hivi nimtimizie kwa nini? La! Ni sharti nitie kikomo. "Hivi tumebaki wawili tu, mbona usigure na kuungana nami kwenye chumba changu?" Alizidi kunieleza. Maneno Haya niliyaona ya utani. Hivi huyu mzee ana akili timamu? Mamangu kazikwa leo tu, na mchangani hajamaliza hata siku, naambiwa nikaridhi chumba chake? Kweli dunia ina mambo.

Sikutaka kuzidi kumskiza kwani alinikera, wala sikuwa tayari kumtimizia matakwa yake, hivyo nikamwomba aondoke. Alisusia na kunivuta kwa nguvu ili niandamane naye. "Nimevumilia ya kutosha! Naomba uniache tena niko radhi nikuondokee hata sasa!" Nilipayuka huku nikijaribu kujinasua kutoka mikononi mwake. Alinizidi nguvu na hatimaye akanirusha kitandani kwake. "Ntaishi hivi mpaka lini? Mungu naomba unipiganie." Nilijiambia kimoyomoyo, ni kweli mnyonge hana haki.

Alijaribu kunishika kwa nguvu nami nikakataa abadan katan kushikamana, ikawa ni vita dhidi ya baba na bintiye kisa mapenzi. Nilinyoosha mkono wangu kwa kutafta kifaa chochote kitakachonisaidia na kwa bahati nzuri nikahisi kifaa chini ya mto. Sikusita kulichomoa ili nijizuie ila nilishtuka kuona kuwa ilikuwa bastola. Alijaribu kunipokonya nami nikajitahidi kulistahimili na katika ile harakati, sijui aliyeibonyeza ni nani, kwani nliskia mlipuko na babangu akawa anavuja damu nyingi ajabu. Lo! Ndio kafa!

Sikujua pa kuanzia, nilichukuwa simu yake ya mkono na kubonyeza nambari ya dharura ili kuwaita polisi. Niliwaeleza kuwa babangu ameaga katika hali ya kutatanisha na wakanihakikishia kuwa watafika kwa takriban muda wa nusu saa. Niliutazama mwili wa babangu kwa majonzi, nilimchukia ndiyo lakini sikunuia kumkatizia maisha yake. Nilipigania uhuru wangu lakini sikutarajia kuvuja damu. Hivi nitawaeleza nini polisi? Ni nani atakayeamini maneno yangu, kuwa babangu alikuwa ananidhulumu kimapenzi na katika hali ya kujiokoa haya yakatokea?

Walitimiza ahadi yao na baada ya nusu saa waliwasili. Walikuwa watano, wanaume wanne na mwanamke mmoja, nami nikawaelekeza hadi chumbani. "Hivi ni nini kilitokea?" Mmoja wao aliuliza. "Ni..liku..wa.....nnaa..ja.ri..bu.." nilishindwa kujieleza nikaishia kwa kilio. Waliukagua mwili na kubaini kuwa alikufa kwa risasi. Ushahidi ulikuwa wazi kuwa hakuna aliyetuvamia na ni mimi ndiye mshukiwa pekee. Niliandamana nao hadi kituo cha polisi, huku mwili wa babangu ukipelekwa katika chumba cha kuhifadhi maiti.

"Msichana mbona ulimuua babako?" Maswali yalizidi, "na bastola ulitoa wapi? Una ruhusa ya kuimiliki?". Yote haya nilijibu kwa kimya, chambilecho wahenga, kimya kingi kina mshindo mkuu. Nilishindwa kabisa kujieleza kwani wengi walimjua babangu kinyume na nilivyomjua mimi. Mamangu pekee ndiye angekuwa wa kuniokoa lakini hayupo tena. Hakukuwa na kesi ya kuskizwa kwani ilikuwa dhahiri kuwa nilimuua babangu, na jela ikawa inanikodolea macho.

Pengine huu ndio uhuru niliotamania, pengine haya ndiyo maisha yatakayonifaa, maisha bila babangu, maisha bila kulawitiwa, maisha gerezani.
picha imedhaminiwa na google.

1 comment:

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...