Tuesday, 26 September 2017

MAJUTO NI MJUKUU

 Azizi Ni kipusa aliyezaliwa na kulelewa kwa njia ya kipekee. Binti huyu mwenye maumbile ya kupendeza na sura nzuri alivutia wengi, wa karibu na mbali, kwenye vitongoji hadi vijiji, wazee kwa vijana, bila shaka alikuwa mfano bora wa binadamu aliyeumbwa akaumbika. Pasi na sura, Azizi alikuwa binti mwenye hulka njema, wengi walimsifia kwa heshima aliyokuwa nayo kwa waliomzidi umri, shuleni alipendwa na walimu, kwani kwenye buku hakuachwa nyuma. Alikua miongoni mwa wanafunzi bora na kila muhula alitunukiwa zawadi chungu furika, ama kweli, Chanda chema huvikwa Pete na mcheza kwao hutuzwa.

Kadri siku zilivyozidi, Azizi naye maisha yake yalianza kubadilika. Alimaliza shule ya upili na kufuzu kwa alama nzuri tu, hivyo akajipa nafasi ya kujiunga na chuo kikuu. Hapo ndipo maisha yake yalianza kufuata mkondo usioeleweka! Au ndio kitumbua kiliingia mchanga? Na kidagaa kumuozea?

Azizi alikuwa si yule Azizi tuliyemjua! Alibadilika na kuwa asiyeambilika wala kusemezeka, hakuskia la mwadhini wala mteka maji msikitini. Wazazi wake walimsikitikia, walimsihi asijekuiga ya dunia na kusahau alikotoka. Walimwonya dhidi ya maisha ya anasa na vijana waso na maana. "Mwanangu chunga, maisha ya ujana yasije yakakuangamiza" Babake alimwonya, ila haya yote yaliangukia sikio la kufa lisilosikia dawa, ama tusema sikio la Azizi alilitia nta kwani yaliingilia kulia na kutokea kushoto.

Ulimwengu ulimkodolea macho kodo! Ulimwita na kumdekeza kwa sana, laiti angalijua masaibu yatakayomkuta! Maskini Azizi! Alijiona kesha fika, mtindo wake wa mavazi ulibadilika, bui bui na mitandio aliyaona ya kishamba na kuwa mwacha mila. Alivaa vijinguo vya kumbana, si vipaipu si mgongo wazi si mini sketi! Binti wa kidijitali! Viatu vya kumuinua juu juu sijui ndio "mkodo mkodo". Alijirembua na kujipodoa kama malkia, hata kipofu angemnusia na kumtamania. Biashara matangazo, naye alijitangaza si haba, kumbuka chema chajiuza, ila yeye aliamua kuwa kibaya cha kujitembeza. Lo! Kaharibikia ukubwani.


"Mwanangu nakupeleka shuleni ukasome. Vyuo vikuu vina majaribio mengi, huko kuna aina zote za raha na karaha, nakuomba uepuke yasokufaa", mama Azizi alimdokezea huku akimdara begani. " I know mum, I'll be fine!" Alijibu Azizi huku macho ameyalegeza kwa mamake. Mamake alimhurumia kwani alikua ameanza kumea pembe tayari, ila aliomba maji yasije yakazidi unga. Alimpeleka mwanawe shuleni na kubaki akimwombea mema huku akiwa na matumaini kuwa mwanawe atazidi kufanya vizuri kwani kwake kupita mitihani Ilikuwa ni sheria kama ibada.



Kama ilivyo ada ya vyuo, wanafunzi wa kike wa mwaka wa kwanza huwa kama ua linalonawiri shambani. Wanafunzi wa kiume hasa wale wenye ufisi huwamezea mate na kuwatamania kutokana na ubichi wao na hivyo huwashambulia na kuwatongoza kwa udi na uvumba, na hapa ndipo wengi hutegwa wakateguka.

Mandhari mapya, maisha mapya na hakuna wakukufwatilizia uko wapi? wafanya nini? na nani? Uhuru ulioje! Maisha hapa ni tofauti kabisa, kudurusu vitabu na kufanya kazi za ziada ni kwa hiari yako. Ni juhudi za mwanafunzi mwenyewe kutumia akili kufanya jambo linalofaa kwa wa wakati unaofaa, kwani hata ingawa wanafunzi wana uhuru huu, mwishowe haya yote huangaziwa ili kumpa mwanafunzi jumla ya alama, mwisho wa semesta, na hapa ndipo wengi hufeli!

Kwa binti Azizi, haya ndiyo maisha aliyoyatamania, maisha bila ratiba. Kufanya unachokitaka bila kunyoshewa kidole wala kelele za mamake za mara kwa mara, raha ilioje! Azizi alijisahau kabisa kama alikua mwanafunzi aliyepelekwa shuleni kusoma, kwake yeye ni kama alikuwa likizo fulani kujistarehesha. Masomo yaligeuka raha iliyokithiri mipaka.

Alijiunga na kundi la wasichana ambao pia waliipa raha kipaumbele. Wote hawa walipoteza mwelekeo wa maisha huku nia yao kuu ikiwa kuutetemesha mtandao na mitindo ya kimavazi, urembo wao na jinsi wanavyojua kuponda raha, yaani "kuparty". Walipiga picha ya kila aina na kuyajaza kwenye akaunti zao za "Facebook" na "Instagram". Waliishi kwa kulewa huku wazazi wao wakidhania kuwa wana wao wako shuleni, na wanasoma kwa manufaa yao ya baadaye, kumbe ndivyo sivyo.

Mapenzi ni kizungu zungu, mapenzi yanaezakufanya ukachanganyikiwa usijue la kufanya. Ni vigumu kutofautisha mapenzi ya dhati na ya ulaghai, ila kwa wengi bora mapenzi, ilimradi moyo umeridhika. Lakini je, ina maana kuwa wana wetu wa vyuo wanafahamu fika maana ya mapenzi? Azizi na kikundi chake walitamaniwa na wengi na katika harakati ya kusumbuliwa na vijana hapa na pale, bila shaka alijikuta kwenye boksi ya Kingi.
Kingi, kijana mtanashati na aliyeunga misuli kama mnyanyua vyuma, aliwazingua mabinti wengi, ila kwa Azizi alifika. Mapenzi yalinoga kwa kiasi cha kumshawishi Azizi kugura kwenye vyumba vya wanafunzi shuleni ili waishi pamoja kwenye chumba cha kukodisha kama mke na mume, haya kama si ya Musa nitayaita ya firauni!




"Beb uko na class leo?"
"Niko na class, but sijiskii kuenda."
Haya ndiyo yalikuwa mazungumzo kati ya hawa wapenzi wawili waliojisahau kuwa ni wanafunzi. Mara nyingi walikuwa wavivu wa kwenda darasani. Walitumia simu zao za rununu kuwasiliana na waliohudhuria masomo ili kujua mambo yalivyokua yakiendelea darasani. Siku ziliyoyoma mtindo ukiwa ni huu huu. Mapenzi yalizidi kunoga, wakala raha zao na pasi kujua, Kingi alifunga bao!

"Mja mzito?" Alimaka mwana wa watu. Hii ni baada ya kujihisi mgonjwa na kujipeleka kwenye zahanati ya shule. Alilazimika kupimwa magonjwa mengi ila uja uzito hakuutarajia kabisa. Nguvu zilimwishia akajiketisha kitako asijuwe pa kuanzia. "Nurse uko sure?" Alimuuliza muuguzi, huku sauti yake ikiwa yenye huzuni tele. Alimwona mamake akiwa amesimama mbele yake, ".....Nakuomba uepuke yasokufaa" aliyakumbuka maneno ya mamake, huku machozi yakimtiririka njia mbili mbili. Alinyanyuka na kujikokota kuelekea chumbani kwao, ili amwelezee mwenzako yaliyowakumba.

Kingi aliipokea habari kwa mshtuko! Alimpenda Azizi ila hakuwa tayari kuitwa baba, la! Suluhisho ni lipi? Yalikuwa yashamwagika na hayangezoleka. Wawili hawa walitofautiana, kwani Kingi alitaka Azizi akaavye mimba lakini yeye hakuwa tayari. Walikorofishana kwa muda huku kila mmoja akimnyooshea mwenzake kidole cha lawama. Kwa kutokubaliana, Azizi alifungasha virago vyake na kumuondokea Kingi. Msururo wa maswali ulimjaa akilini akose wa kumjibu. Alitamani dunia ipasuke na kummeza mzima mzima, kwani alijihisi si wa maana tena.

Azizi alijikuta katika hali ngumu mno. Mitihani ilikaribia, marafiki walimtenga na wazo la kuwa mama mtarajiwa lilikuwa kama jinamizi. Aligeuka na kuwa gumzo la wengi pale shuleni. Waliyomwonea gere walimsimanga huku wengine wakimuonea huruma. Mwana wa watu alinyong'onyea, alitamana yote haya yawe ni ndoto, na kuwa ataamka na kurudia maisha yake ya zamani. Alitamana miujiza ifanyike, wakati urudi nyuma ili arekebishe alipokesea, lakini ng'o! aliangulia pang'anda. Lisilo budi hubidi, Naye hakuwa na budi ila kukubali yaliyomfika.

Kutokana na kutohudhuria kwake kwa masomo, Azizi hakuweza kujiandaa vilivyo kwa mitihani. Aliamua liwe liwalo, na kukosa kufanya mtihani huo. Alikuwa ashateleza na kwake yeye ule uja uzito ulimpa stresi zaidi ya chochote kile. Mitihani ilikamilika na wakati wa likizo ukawa umetimia. Hakutamani kabisa kwenda nyumbani, kwani babake ni simba, tena mwenye ghadhabu ajabu. "Hivi nitaenda kwa nani? Nitamweleza nini babangu?" Aliwaza.


No comments:

Post a Comment

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...