Tuesday 3 October 2017

ALIDHANI ZEZETA KUMBE KAMZIDI AKILI.

Bwana Dzombo ataishi kwa kumbumbu ya maisha ya usukule aliyopitia mikononi mwa Mayasa. Wala sidhani kama atajikuta katika hali ya kumtamania mke mwingine kando na mkewe. Maisha ya udanganyifu katika ndoa, maisha ya mpango wa kando yaani mchipuko, basi ndio kakoma!

Miaka miwili iliyopita, bwana Dzombo alibahatika kupata nafasi ya kujiendeleza kimasomo nje ya nchi, ili apate ongezeko la cheo (promotion) anapofanya kazi. Wakati huu mkewe alikuwa ni mja mzito na hivyo wakakubaliana kumtafta binti wa kazi kwani hangeweza kujidhibiti katika hali yake. Mke wa watu alijitahidi kutafta na mwishowe akampata Mayasa, binti mchafumchafu ambaye ungemfananisha na zezeta fulani.

Baada ya kumkagua, Dzombo aliridhishwa naye kwani hakuonekana mwenye madhara hata kwa ndugu zake wa kiume ambao huwatembelea mara kwa mara, kutokana na hali yake duni. Kwa makubaliano, Mayasa alijitolea kuwafanyia kazi naye Dzombo na mkewe wakaahidi kumsaidia ili ajiendeleze kimasomo. Mipango ilikamilika, Dzombo akasafiri na mkewe akabaki salama salimini.

Alienda kwa muda wa takriban mwaka mmoja na nusu hivi, na baada ya kukamilisha masomo yake, muda wake wa kurejea ukawadia. Aliporudi, mkewe alikuwa amesafiri kijijini hivyo akamsihi dadake, ambaye anaishi mtaa jirani na wanapoishi, aende kumpokea. Alipofika nyumbani kwake, alishangaa kumwona mgeni. Dzombo alipokelewa na kipusa mrembo ajabu, tena mwenye umbo la kutamaniwa na wengi. "Hivi ni nani huyu aliyetupokea?" Alimuuliza dadake. "Si ni Mayasa yule...." Alijibiwa. "Mayasa? Mbona kabadilika haraka vile?" Alizidi kushangaa.

Mabadiliko ya Mayasa yalimsababishia Dzombo kumtamania kwa sana. Alipiga moyo konde na kujaribu kujizuia lakini wapi, tamaa ilimzidi na mwishowe akamwaga radhi. "La! Haiwezekani, tena mkeo namheshimu na kumchukulia kama dadangu kwa mengi mema aliyonitendea, hivyo siwezi kumkosea. Naomba usahau, kwani kwangu utazidi kuwa kaka." Ndiyo majibu aliyoyapata Dzombo baada ya kumtongoza Mayasa. Alibaki kwa kujutia kitendo chake cha kijinga.

Siku iliyofwata, mzee wa watu alikuwa kajiketisha sebuleni kwa mapumziko na mawazo, akapita Mayasa kutoka hamamuni kuelekea chumbani kwake, tena nguo hana, kajibwagia kanga tu. Dzombo kwa kumtazama, alishindwa kujistahimili, hisia zikampanda na akamfwata Mayasa. Mara hii aliweza kutembea naye, ila baada ya tukio, Mayasa alimhakikishia kuwa atajuta. Alijiona mjanja na kuyapuuza maneno ya Mayasa, kwani aliyaona kuwa ya vitisho tu.

Waliishi kwa kutosemezana kwa siku kadhaa kila mmoja akifwata shughuli zake, lakini mambo yakabadilika Dzombo alipogundua kuwa nguo zake za ndani zilikuwa zinakosekana. Alitafta kila pembe na mwishowe akaelekea chumbani kwa Mayasa. Katika harakati ya kupekuapekua hakuamini macho yake alipoona nguo yake moja ya ndani imefungwa na kitambaa chekundu na katikati ina nywele, moyo wake ulisimama ghafla. "Mayasaaaa!!!!" Aliita kwa hasira. Alimwita ili aeleze nini maana ya kile alichokiona. "Babu yangu alinionya dhidi ya kulala na mtu yeyote, hadi pale atakaponioa na kunilipia mahari. Hivyo baada ya kumwelezea ulichonifanyia, aliniagiza nimsafirishie nguo zako za ndani." Alieleza mdada. Dzombo alitoneshwa kidonda, "naomba uziregeshe haraka au nitakufungaaa!" alifoka. "Naomba ukinifunga, umfunge na babu yangu maana nawe uko kifungoni." Mayasa alimalizia.

Dzombo alijihisi msukule, alijikuta chooni bila kufahamu. Haidhuru, alijiketisha pale ili angalau ajisaidie. Dakika zilipita kama kumi na tano hivi, hakuna kitu! "Ala! Kwani babu keshaanza mazingaombwe yake?" Alijiuliza. Aliondoka nyumbani kwake na kuelekea katika baa moja mtaani ili kupunguza mawazo kwa chupa mbili tatu. Akiwa pale, alimpigia mkewe simu ili kujua mengi kumhusu Mayasa. " Hivi anatokea wapi huyu Mayasa?" Aliuliza katikati ya mazungumzo. "Si ni wa Msambweni yule, mbona wauliza?" mkewe alijibu. "MSAMBWENI?" Dzombo alishtuka nusura apaliliwe na pombe. "Hivi haezi kuwa na mambo ya kichawi mdigo yule? Anamlea mwana wetu kumbuka" Alimweleza mkewe kwa kukosa jibu mwafaka kuhusiana na mshtuko wake.

Aliacha pombe na kurejea nyumbani ili amwombe msamaha kijakazi wake. Mayasa alikataa, tena baya zaidi alidokeza kuwa alikuwa anamsubiri mkewe arudi ili amwelezee yaliyowakumba kuondoa lawama kwa litakalotokea. Dzombo alijutia na kuhofia ndoa yake. Alimkemea shetani aliyemdanganya na kumwingia mpaka akatembea na Mayasa. Lakini ni shetani kweli wanavyodai wengi, au tamaa tu za kimwili?

Mkewe aliporudi, Dzombo hakuwa na amani ila alijizui mkewe asije akagundua. Alifurahi sana kumwona mwanawe hata akapanga kuwapeleka matembezi kama familia wakajivinjari. Mpango huu ulipanguliwa na Mayasa. Dzombo alimkuta jikoni Akifanya kazi zake za kawaida na kumwia radhi, "Babu yangu anauliza una mpango gani na mimi? Au aendelee na taratibu zake?" Maneno haya ya Mayasa yalizidi kumkosesha raha. Aliwaza na mwishowe akaamua kumhonga.

Alichukua shilingi elfu hamsini pesa taslimu na kumkabithi Mayasa. Mayasa alipokea kifurushi kile cha pesa na kuelekea chumbani kwake. Baada ya muda, Dzombo alishtuka kuregeshewa hela zake huku zimefungwa na hirizi. "Elfu hamsini yaeza fanya nini katika maisha ya sasa?" Mayasa alimuuliza kwa dharau, chambilecho wajadi, zimwi likujualo, halikuli likakwisha.

Dzombo alishikamana, alimpenda sana mkewe na hakutaka vurugu kwenye ndoa yake. Aligharamika na kumwondoa Mayasa nyumbani kwake kwa kumfungulia biashara ya duka la vipodozi. Mayasa alitoshelezeka hatimaye na kumshukuru sana Dzombo. "Asante sana kaka, wala usitie shaka maana hakuna ushirikina wowote nilitia juu yako." Mayasa Alimweleza. Dzombo alijihisi mjinga, tena baada ya kujitia hamnazo na kugharamika vile ili kukwepa uchawi. La haula, pwagu kampata pwaguzi.
Dzombo akijutia kitendo chake.
picha imedhaminiwa na facebook.

No comments:

Post a Comment

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...