Wednesday, 25 April 2018

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu
Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu
Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie

Kitizama likotoka, hatua mepiga Sana
Katika vyombo tajika, kazi yako tumeona
Citizeni bila Shaka, wapambia kama hina
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Sauti yako nyororo, Kama chatu navutiwa
Katika giza totoro, niondowe Kama njiwa
Wanionao kiporo, Washtuke kipakuliwa
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Taka huo ujasiri, taka huo ubunifu
Kwenye kamera si siri, kazi ngumu ya kusifu
Nataka kuwa mahiri, Kama wewe mkufuu
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Tafurahi kitimiza, ndoto yangu aushini
Ninaapa kutocheza, funzo lako tathamini
Niinue Kama pweza, nyayo zako natamani
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Lulu jina Kama ua, nipambie ari yangu
Hasani mama tambua, taka uwe ngao yangu
Maza Aziza najua, kazi zako hizi tangu
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Natumai mesikia, ombi langu la moyoni
Siriyo natamania, ila bado ni taabani
Kama vile abiria,  lako gari niko ndani
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.
Lulu Hassan.

TATU MWAKA TUMEFIKA

Kikumbuka likotoka, mie chozi lanilenga
Japo mimba lipachika, kulikuza kajitenga
Muda bado, alimaka, tulitoe aliunga
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Kwangu likuwa zawadi, kwa dhati lisubiria
Japo shida ilizidi, Kwa Mola liangazia,
Uzazi kwangu libidi, Hata shule kuachia
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Ni mbali kifikiria, tumetoka na mwanangu
Hata njaa kilalia, kwa kuzongwa na machungu
Ma' mkwe kasaidia, pokea shukrani zangu
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Mwana ukizidi kua, mema mengi zingatia
Heshima kwako tambua, kote kote angazia
Wako baba keshajua, ndiwe wake malkia
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Japo baba nami mama, kisogo lishapeana
Kwako mwana tulisema, takulea kwa kufana
Hakikisho la kusoma, tatimiza na kwa sana
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Sasa natia kikomo, tamati ya simulizi
Mwana menipa kisomo, cha maisha wazi wazi
Tatu mwaka siwe shimo, mengi mema na yazidi
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Monday, 26 February 2018

MAKOVU YA STAHAMALA

picha ya Galma Boru





Je, ni nini haswa kilichochangia kijana huyu kuliasi dini la kiislamu na kuwa mkristo katika kanisa la 'Good News Mission'? Hili ni swali tata nililojiuliza mno baada ya kumsikiza  akitoa ushuhuda wa wokovu wake katika moja wapo ya ibada katika kanisa kuu la Good News Mission jijini Nairobi. Kama vile fisi, nilijawa na tamaa ya kutaka kujua mengi kuhusu kijana huyu, hivyo nikamtafuta hususan kwa  majadiliano, ili niweze kutuliza kiu yangu ya kutaka kujua mengi kumhusu.
"Ndugu zangu wa toka nitoke walinipiga vita, walipogundua kuwa naenda kanisani, maana katika familia yetu tulizaliwa katika dini ya kiislamu", ndiyo maneno yaliyonipa ari ya kutaka kuelewa fika, ni nini kiini cha yeye kufika kanisani?

Galma Boru, ni kijana mwenye asili ya kiborana. Chimbuko lake ni la nchi jirani ya Ethiopia, ila kupitia mateso ya vita nchini humo,babake mzazi alijitia mhanga na kutorokea nchni Kenya katika eneno la Moyale, hivyo Galma akapata kuzaliwa katika eneo hili. Wakaazi wa eneo la Moyale wana makovu ya dhiki, baada ya kubanwa na madhila kama tai si haba, si vita, si njaa. Ikumbukwe, katika miaka ya nyuma (2011-2012) wakaazi hawa wa Moyale katika kaunti ya Marsabit walikumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha watu wengi kuachwa bila makao. Wengi walipoteza maisha yao huku wengine wakiamulia miguu niponye na  kutorokea mpakani nchini Ethiopia na sehemu zingine ili kuokoa maisha yao. Taswira hii, anaikumbuka Galma utadhani tukio la jana, kwani aliponea kifo chupu chupu.

"Sisi tulibebwa na lori, katika hali mbaya sana. Tulibanana na mifugo mle ndani kusudi tuweze kutoroka na kuyaokoa maisha yetu. Njiani kulikuwa na milio ya risasi, nami niliweza kushuhudia vifo vya watu wengi, ila kwangu mimi, Maulana alinirehemu nikawa mmoja wa wale waliyobahatika kufika salama salimini", Galma alizidi kunidokezea.

Kwa muhtasari, ni mengi aliyopitia ghulamu huyu hata akapata kufika Athi River kaunti ya Machakos, wanakoishi sasa jamaa zake, lakini linalomtonesha kidonda mpaka sasa ni kuugua kwa mamake. Alinieleza kuwa ninake ameugua kwa muda mrefu pasi na kupata matibabu ya kutia kikomo mateso anayoyapitia. Mamake anaugua ugonjwa wa kiakili na amepelekwa mara nyingi katika hospitali kuu ya rufaa ya Mathare, ila mpaka sasa hawajapata matibabu kamili. Hali hii tatanishi ya mamake ilimghabisha mno Galma, laiti angalikuwa na uwezo, kwani kwake yeye anahisi kuwa huenda pengine mamake anapitia dhiki hizi kwa kukosa mtu wa kumwelea, mtu wa kumdekeza na kumpa mapenzi na pengine kumwondoa katika maisha ya dhiki kwani yote haya huenda yakawa ndiyo chanzo cha ugonjwa wake. Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki, huenda kwa nina huyu, hana mwendani hata mmoja, kwani aliyemdhania kuwa rafiki wake wa karibu, pia amebaki kumpa kibwagizo cha lawama na kumwona kama mzigo na asiyekuwa na manufaa yoyote. Ada ya mja hunena, mungwana ni kitendo, bila shaka, amekosa wa kumtendea, na kubaki na wa kumtenda tu!

Kila mja na bahati yake, katika pita pita za Galma, siku mosi huko maeneo ya Kitengela, aliweza kuona bango lenye matangazo ya huduma za bure za matibabu. Alisahau shughuli zilizomfikisha eneo hilo na kutaka kujua zaidi kuhusu huduma hizi, ili kujua iwapo mamake angepata afueni mahala pale. Aliagizwa kuenda siku iliyofuata naye akatii amri, hivyo akamfikisha mamke pale kulingana na maagizo. Huduma hii ya matibabu ilikuwa imedhaminiwa na kanisa la Good News Mission, na hivyo hapa ndipo kwa mara ya kwanza kabisa alipata kuskia habari njema ya Yesu Kristo, na kama vile chatu pangoni, aliweza kuvutiwa na akawa na hamu ya kutaka kujua zaidi.

Siri ya msamaha wa dhambi, ujumbe wa kutakaswa na kufanywa mtakatifu na mkamilifu, hisia ya kuwa mwana wa Mungu na ufahamu wa kuwa analindwa naye Mwenyezi, na kuwa shida zake zote anazifahamu Maulana na atamsaidia pasi na yeye kufanya lolote, ila tu kuamini, Galma alikuwa mwenye furaha ghaya. Alihisi wepesi moyoni mwake na kuamua kumfuata huyu Mungu aliyemhakikishia maisha ya milele.
 
Galma na kundi la vijana la IYF, katika kambi kubwa
 ya vijana duniani alimaarufu, "IYF World Camp"
mwaka 2017.

"Mimi nina furaha kuishi kanisani, na hawa ndugu na dada wa kanisani ndio ndugu na dada zangu. Hata ingawa baadhi ya jamaa zangu wananipiga vita kuwa hapa, sijali maana Mungu amenipa familia nyingine," alimalizia. Penye nia pana njia, nia yake ya kutaka kujua zaidi kuhusu mafunzo ya Bibilia hata baada ya kupigwa vita, ilimfikisha kanisani. Aliamua liwe liwalo na kugura kutoka kwao ili kuishi kanisani, hapa alijiunga na kundi la vijana la IYF (International Youth Fellowship) , ambalo lina mikakati mengi ya kuwainua vijana kupitia mafunzo mengi ikiwemo mafunzo ya kiakili (Mind Set).

Simulizi la ghulamu huyu lilinipa mafunzo mengi, makovu ya stahamala aliyoyapitia yalimfungulia njia za baraka, kwani hivi sasa, Galma yuko katika kituo cha televisheni cha GBS kujifunza chochote kile anahisi angependa kujua katika ulimwengi wa uwanahabari na vyombo vyake. Raha iliyoje!
Galma, katika kituo Cha
 televisheni Cha GBS.



Tuesday, 13 February 2018

WEMA WA KUOZA?


Siku nenda siku rudi, tunashuhudia sakata ya makali ya kiangazi na njaa nchini pasi na matumaini ya kupata suluhisho la kudumu. Vyombo vya habari hutupa taswira ya kutamausha kwa kuangazia swala nyeti la kiangazi na baa la njaa.  Ni utu au uhayawani, tunapowakodolea macho kodo waathiriwa wa njaa huku tukila na kusaza? 
Image result for baa la njaa africa   
Image result for baa la njaa africaMaeneo ya Wajir, Baringo, Kilifi na maeneo mengine mbalimbali katika mkoa wa Kaskazini na Kaskazini Mashariki ni baadhi ya maeneo ambayo yameadhirika pakubwa kutokana na uhaba wa chakula. Wakaazi wa maeneo haya hukodolea kifo macho kwa kukosa hitaji la msingi mno (chakula). Je, maskini hawa wa Mungu wako katika dunia nyingine au hii moja wanaoishi mabwenyenye? Ahadi ya serikali ya kuwapa tumaini la kuishi walala hoi hawa litatimia lini?

Wana nyuso za kusikitisha, miili yao iliyokonda na kukondeana pia ni ya kughadhabisha, lakini nani wa kuwasaidia? Lisilobudi hubidi, na wao hawana budi ila kuamka kila uchao na kupambana na hali yao huku wakiwa na matumaini ya kupata afueni katika siku za usoni au kupitia kwa wasamaria wema. Huenda siku moja Maulana atafanya miujizi na masaibu wanayopitia waja hawa  yatatokomea milele, kwani serikali inayopaswa kuwajali, haijali togo wala jando. Ni wengi wamepoteza maisha yao, na kuwa kitoweo cha mauti, kwa ukosefu wa chakula. La haula!, sheria ya maskini haiko katika serikali ya mwenye navyo.

Mashirika yasiyo ya kiserikali alimaarufu (NGO's) kwa lugha ya kimombo, yamekuwa katika mstari wa mbele kwa kusaidia mikasa kama hii. Mashirika haya ambayo sana sana huwategemea wasamaria wema ili kutoa misaada yao, hujizatiti mno kwa kutoa huduma zao. Juhudi ambazo iwapo serikali ingeweza kuiga, basi majanga kama haya yangekuwa nadra sana. Cha kusikitisha ni kuwa, serikali ina uwezo mkubwa wa kuwasaidi maskini hohehahe hapa nchini, zaidi ya mashirika haya ya kibinafsi, ila ubinafsi na ufisadi uongozini, umesababishia kuwasahau wahusika wakuu wanaohitaji fedha za serikali.

Kila mwaka, bajeti inapotolewa, pesa hutengwa kwa mikakati ya sekta mbalimbali serikalini. Pesa hizi ni pamoja na pesa za kusaidia kukabiliana na majanga kama haya ya njaa na ukame nchini. Swali ni je, pesa hizi hutimiza kazi zilizokusudiwa au huishia mifukoni mwa watu binafsi?

Viongozi wetu wanapotoa misaada kwa majanga kama haya, wao huyafanya yaoneka kana kwamba ni jambo la kustaajabisha au kuvuliwa kofia. Wengi hujipigia debe na kujipiga kifua ili waonekane wachapa kazi, lakini ukweli ni kuwa, sivyo tudhaniavyo sisi. Katika asilimia mia ya pesa wanazopewa kuwasaidia watu mashinani, aslimia zaidi huishia katika mifuko yao. Kiwango cha msaada wanaotoa ni kidogo ghaya, na wakati wanapotoa wao huandamana na wanahabari na kujaza picha mitandaoni ili kuanikia wakenye jinsi walivyo wachapa kazi, ukweli ukiwa ni kinyume. Msaada wa hakika hauhitaji matangazo, sio lazima ugonge vichwa vya habari ndio uonekane kama msaada, kumbuka zuri chajiuza, kibaya chajitembeza.

Waswahili walinena kuwa, tenda wema nenda zako, wakaja wakaongeza kuwa, wema hauozi, lakini wema wa serikali yetu pamoja na uongozi wake ni wema wa aina gani? Ni wema huu, au uozo na unyama? Mtu mwenye akili timamu na mwenye utu ya binadamu anaweza kuwakodolea macho watu wanaokufa kutokana na njaa, ilhali pesa zinazostahili kuwasaidia, anajilimbikizia na kujiendelezea utajiri? Si huu ndio uhayawani aliyoimba msanii Nyashinski? Si haki kabisa!

    Image result for makali ya kiangazi afrika



Wednesday, 31 January 2018

KARIBU DUNIANI

Kupitia somo la kisayansi la Bayolojia, tunaelewa fika kuwa, pindi tu yai la mume linapokutana na yai la mke, iwe ni wakati wa kitendo cha ndoa au la, basi hapo ndipo maisha ya kiumbe chochote kile chenye uhai huanza. Binadamu ni kiumbe ambaye maisha yake ni ya dhamana mno, lakini ukweli ni kuwa wengi wetu tuko hapa duniani kupitia neema ya Mwenyezi Mungu, kwani wana wengi hukufu kabla au hata wakati wa kuzaliwa, sababu zikiwa ni chungu furika.


Lusaka, Zambia. Very pregnant young African woman in ragged clothes outside her poor house on the outskirts of the - Stock Image
 binti mdogo mjamzito
kimedhaminiwa na google
 Uja uzito ni hali ambayo hukumbwa na hali ya sintofahamu na mabadiliko mengi ya kimaumbile. Habari ya kuwa mama mtarajiwa hupokelewa katika hali tofauti tofauti kulingana na jinsi mtu alivyojipanga au hali yake ya maisha. Katika karne ya saa, tunao mabinti wengi ambao hupachikwa mimba wakiwa bado katika umri mdogo. Je, ni vipi mabinti hawa hukidhi hali hii? Wengi wao hulazimika kuavya huku wachache wanao stahimili wakati huu mgumu, hujifungua kupitia shida nyingi ajabu. Safari ya kukaribishwa duniani, je, atafika akiwa hai au maiti? Atafika katika hali ya raha au shida? Atazaliwa hospitalini au atatupwa chooni?

Maisha ya ufukura imesababishia vifo vya watoto wengi kabla ya kuzaliwa au hata wakati au baada ya kuzaliwa. Hata ingawa maisha ya wanawake wajawazito imezidi kuboreshwa, kupitia uanzilishi wa 'Linda Mama Boresha Jamii," inayotoa huduma za bure kwa kina mama waja wazito katika hospitali  za serikali, huduma hizi hazisaidii aslilimia mia ya wanawake. Suluhisho la asilimia mia ni lipi? sidhani nina jibu, ila nawasikitia kina mama ambao wanakumbana na shida hizi, kwani wengi pia hupoteza maisha yao hasa wakati wa kujifungua.

Iwapo wewe ni mzaliwa wa jijini, shukuru Mungu. Iwapo eneo lenu au hata bara kwenu kuna hospitali, na huduma zinapatikana kwa urahisi, basi wewe ni mmoja wapo wa wale wenye bahati nasibu. Tunao adinasi wengi wanaoishi katika maeneo ya kusikitisha sana. baadhi ya maeneo haya ni kama vile sehemu nyingi za kaskazini mashariki. Eneo hizi zina hospitali chache sana za serikali na barabara pia ni duni ajabu, hivyo kuwasababishia wanaoishi mbali kushindwa kufika hospitalini ili kupata matibabu. Je, tatizo hili laweza kutatuliwa na nani kama si serikali? Ahadi tunazo, lakini ngoja ngoja itazidi kutuumiza matumbo, huku watoto wengi wakikaribishwa duniani na kifo.

Mama mja mzito anapaswa kuenda hospitalini takriban kila mwezi ili kuangaliwa iwapo kitoto chake tumboni kinakua salama salimini, au iwapo ana ugonjwa wowote ili kuelekezwa ipasavyo. Katika maeneo ambayo hospitali ni chache na kuna ugumu wa kuyatembelea kutokana na umbali na barabara mbovu, wanawake wengi huamua kuwatembelea wakunga wenye ujuzi ili wasaidike. Wakunga hawa hutumia miti shamba kutokana na itikadi zao za kitamaduni. Mbinu hizi huhatarisha maisha ya mama pamoja na kitoto chake tumboni na hivyo huchangia pakubwa katika vifo vya mama wajawazito au watoto wachanga. Na hivi ndivyo wanavyo karibishwa duniani baadhi ya wana wetu.


Pregnant african woman with child, Madagascar - Stock Image  
mama mjamzito katika eneo duni.
kimedhaminiwa na google



Hiki ni kilio, hiki ni kilio changu na natumai pia ya wale wenye macho ya kuweza kuyaona niyaonayo mimi. kwenye mizani, sijui waweza kuipa serikali uzito upi katika kuangalia maslahi ya kina mama waja wazito, hasa katika haya maeneo duni yaliyojaa walala hoi, wale tuwaitao 'maskini hohehahe.' ? 

Sote ni waathiriwa kwa njia moja au nyingine, kina mama hawa ni jamaa zetu. Sio tu katika maeneo haya, bali nchi nzima inakumbana na shida nyingi katika kuwahudumia kina mama wajawazito. Ufisadi uongozini umekithiri mipaka na kuzorotesha utoaji huduma. Leo hii, idadi ya kina mama katika wadi za kujifungua imeongezeka maradufu, ilhali vifaa ni vile vile(vichache mno). Dawa hazipatikani hospitalini na mara nyingi wagonjwa hulazima kununua dawa katika maduka ya dawa ambayo sana sana zinamilkiwa na wahudumu wa hospitalini, hasa madaktari wenye vyeo kubwa kubwa. Ndiyo huduma ya bure hii, au vipi?


Heko kina mama wote! nawavulieni kofia kwa mengi magumu mliyoyapitia ili kuwafikisha wana duniani. bila shaka tumeijaza alivyoamuru Mwenyezi Mungu. Shukuru ulivyopokelewa duniani, maana ni wengi dunia hii waliionea paa!


Image result for pictures of poor facilities of giving birth in africa
karibu duniani.
kimedhaminiwa na google.

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...