Monday 26 February 2018

MAKOVU YA STAHAMALA

picha ya Galma Boru





Je, ni nini haswa kilichochangia kijana huyu kuliasi dini la kiislamu na kuwa mkristo katika kanisa la 'Good News Mission'? Hili ni swali tata nililojiuliza mno baada ya kumsikiza  akitoa ushuhuda wa wokovu wake katika moja wapo ya ibada katika kanisa kuu la Good News Mission jijini Nairobi. Kama vile fisi, nilijawa na tamaa ya kutaka kujua mengi kuhusu kijana huyu, hivyo nikamtafuta hususan kwa  majadiliano, ili niweze kutuliza kiu yangu ya kutaka kujua mengi kumhusu.
"Ndugu zangu wa toka nitoke walinipiga vita, walipogundua kuwa naenda kanisani, maana katika familia yetu tulizaliwa katika dini ya kiislamu", ndiyo maneno yaliyonipa ari ya kutaka kuelewa fika, ni nini kiini cha yeye kufika kanisani?

Galma Boru, ni kijana mwenye asili ya kiborana. Chimbuko lake ni la nchi jirani ya Ethiopia, ila kupitia mateso ya vita nchini humo,babake mzazi alijitia mhanga na kutorokea nchni Kenya katika eneno la Moyale, hivyo Galma akapata kuzaliwa katika eneo hili. Wakaazi wa eneo la Moyale wana makovu ya dhiki, baada ya kubanwa na madhila kama tai si haba, si vita, si njaa. Ikumbukwe, katika miaka ya nyuma (2011-2012) wakaazi hawa wa Moyale katika kaunti ya Marsabit walikumbwa na vita ya wenyewe kwa wenyewe iliyosababisha watu wengi kuachwa bila makao. Wengi walipoteza maisha yao huku wengine wakiamulia miguu niponye na  kutorokea mpakani nchini Ethiopia na sehemu zingine ili kuokoa maisha yao. Taswira hii, anaikumbuka Galma utadhani tukio la jana, kwani aliponea kifo chupu chupu.

"Sisi tulibebwa na lori, katika hali mbaya sana. Tulibanana na mifugo mle ndani kusudi tuweze kutoroka na kuyaokoa maisha yetu. Njiani kulikuwa na milio ya risasi, nami niliweza kushuhudia vifo vya watu wengi, ila kwangu mimi, Maulana alinirehemu nikawa mmoja wa wale waliyobahatika kufika salama salimini", Galma alizidi kunidokezea.

Kwa muhtasari, ni mengi aliyopitia ghulamu huyu hata akapata kufika Athi River kaunti ya Machakos, wanakoishi sasa jamaa zake, lakini linalomtonesha kidonda mpaka sasa ni kuugua kwa mamake. Alinieleza kuwa ninake ameugua kwa muda mrefu pasi na kupata matibabu ya kutia kikomo mateso anayoyapitia. Mamake anaugua ugonjwa wa kiakili na amepelekwa mara nyingi katika hospitali kuu ya rufaa ya Mathare, ila mpaka sasa hawajapata matibabu kamili. Hali hii tatanishi ya mamake ilimghabisha mno Galma, laiti angalikuwa na uwezo, kwani kwake yeye anahisi kuwa huenda pengine mamake anapitia dhiki hizi kwa kukosa mtu wa kumwelea, mtu wa kumdekeza na kumpa mapenzi na pengine kumwondoa katika maisha ya dhiki kwani yote haya huenda yakawa ndiyo chanzo cha ugonjwa wake. Akufaaye kwa dhiki ndiye rafiki, huenda kwa nina huyu, hana mwendani hata mmoja, kwani aliyemdhania kuwa rafiki wake wa karibu, pia amebaki kumpa kibwagizo cha lawama na kumwona kama mzigo na asiyekuwa na manufaa yoyote. Ada ya mja hunena, mungwana ni kitendo, bila shaka, amekosa wa kumtendea, na kubaki na wa kumtenda tu!

Kila mja na bahati yake, katika pita pita za Galma, siku mosi huko maeneo ya Kitengela, aliweza kuona bango lenye matangazo ya huduma za bure za matibabu. Alisahau shughuli zilizomfikisha eneo hilo na kutaka kujua zaidi kuhusu huduma hizi, ili kujua iwapo mamake angepata afueni mahala pale. Aliagizwa kuenda siku iliyofuata naye akatii amri, hivyo akamfikisha mamke pale kulingana na maagizo. Huduma hii ya matibabu ilikuwa imedhaminiwa na kanisa la Good News Mission, na hivyo hapa ndipo kwa mara ya kwanza kabisa alipata kuskia habari njema ya Yesu Kristo, na kama vile chatu pangoni, aliweza kuvutiwa na akawa na hamu ya kutaka kujua zaidi.

Siri ya msamaha wa dhambi, ujumbe wa kutakaswa na kufanywa mtakatifu na mkamilifu, hisia ya kuwa mwana wa Mungu na ufahamu wa kuwa analindwa naye Mwenyezi, na kuwa shida zake zote anazifahamu Maulana na atamsaidia pasi na yeye kufanya lolote, ila tu kuamini, Galma alikuwa mwenye furaha ghaya. Alihisi wepesi moyoni mwake na kuamua kumfuata huyu Mungu aliyemhakikishia maisha ya milele.
 
Galma na kundi la vijana la IYF, katika kambi kubwa
 ya vijana duniani alimaarufu, "IYF World Camp"
mwaka 2017.

"Mimi nina furaha kuishi kanisani, na hawa ndugu na dada wa kanisani ndio ndugu na dada zangu. Hata ingawa baadhi ya jamaa zangu wananipiga vita kuwa hapa, sijali maana Mungu amenipa familia nyingine," alimalizia. Penye nia pana njia, nia yake ya kutaka kujua zaidi kuhusu mafunzo ya Bibilia hata baada ya kupigwa vita, ilimfikisha kanisani. Aliamua liwe liwalo na kugura kutoka kwao ili kuishi kanisani, hapa alijiunga na kundi la vijana la IYF (International Youth Fellowship) , ambalo lina mikakati mengi ya kuwainua vijana kupitia mafunzo mengi ikiwemo mafunzo ya kiakili (Mind Set).

Simulizi la ghulamu huyu lilinipa mafunzo mengi, makovu ya stahamala aliyoyapitia yalimfungulia njia za baraka, kwani hivi sasa, Galma yuko katika kituo cha televisheni cha GBS kujifunza chochote kile anahisi angependa kujua katika ulimwengi wa uwanahabari na vyombo vyake. Raha iliyoje!
Galma, katika kituo Cha
 televisheni Cha GBS.



Tuesday 13 February 2018

WEMA WA KUOZA?


Siku nenda siku rudi, tunashuhudia sakata ya makali ya kiangazi na njaa nchini pasi na matumaini ya kupata suluhisho la kudumu. Vyombo vya habari hutupa taswira ya kutamausha kwa kuangazia swala nyeti la kiangazi na baa la njaa.  Ni utu au uhayawani, tunapowakodolea macho kodo waathiriwa wa njaa huku tukila na kusaza? 
Image result for baa la njaa africa   
Image result for baa la njaa africaMaeneo ya Wajir, Baringo, Kilifi na maeneo mengine mbalimbali katika mkoa wa Kaskazini na Kaskazini Mashariki ni baadhi ya maeneo ambayo yameadhirika pakubwa kutokana na uhaba wa chakula. Wakaazi wa maeneo haya hukodolea kifo macho kwa kukosa hitaji la msingi mno (chakula). Je, maskini hawa wa Mungu wako katika dunia nyingine au hii moja wanaoishi mabwenyenye? Ahadi ya serikali ya kuwapa tumaini la kuishi walala hoi hawa litatimia lini?

Wana nyuso za kusikitisha, miili yao iliyokonda na kukondeana pia ni ya kughadhabisha, lakini nani wa kuwasaidia? Lisilobudi hubidi, na wao hawana budi ila kuamka kila uchao na kupambana na hali yao huku wakiwa na matumaini ya kupata afueni katika siku za usoni au kupitia kwa wasamaria wema. Huenda siku moja Maulana atafanya miujizi na masaibu wanayopitia waja hawa  yatatokomea milele, kwani serikali inayopaswa kuwajali, haijali togo wala jando. Ni wengi wamepoteza maisha yao, na kuwa kitoweo cha mauti, kwa ukosefu wa chakula. La haula!, sheria ya maskini haiko katika serikali ya mwenye navyo.

Mashirika yasiyo ya kiserikali alimaarufu (NGO's) kwa lugha ya kimombo, yamekuwa katika mstari wa mbele kwa kusaidia mikasa kama hii. Mashirika haya ambayo sana sana huwategemea wasamaria wema ili kutoa misaada yao, hujizatiti mno kwa kutoa huduma zao. Juhudi ambazo iwapo serikali ingeweza kuiga, basi majanga kama haya yangekuwa nadra sana. Cha kusikitisha ni kuwa, serikali ina uwezo mkubwa wa kuwasaidi maskini hohehahe hapa nchini, zaidi ya mashirika haya ya kibinafsi, ila ubinafsi na ufisadi uongozini, umesababishia kuwasahau wahusika wakuu wanaohitaji fedha za serikali.

Kila mwaka, bajeti inapotolewa, pesa hutengwa kwa mikakati ya sekta mbalimbali serikalini. Pesa hizi ni pamoja na pesa za kusaidia kukabiliana na majanga kama haya ya njaa na ukame nchini. Swali ni je, pesa hizi hutimiza kazi zilizokusudiwa au huishia mifukoni mwa watu binafsi?

Viongozi wetu wanapotoa misaada kwa majanga kama haya, wao huyafanya yaoneka kana kwamba ni jambo la kustaajabisha au kuvuliwa kofia. Wengi hujipigia debe na kujipiga kifua ili waonekane wachapa kazi, lakini ukweli ni kuwa, sivyo tudhaniavyo sisi. Katika asilimia mia ya pesa wanazopewa kuwasaidia watu mashinani, aslimia zaidi huishia katika mifuko yao. Kiwango cha msaada wanaotoa ni kidogo ghaya, na wakati wanapotoa wao huandamana na wanahabari na kujaza picha mitandaoni ili kuanikia wakenye jinsi walivyo wachapa kazi, ukweli ukiwa ni kinyume. Msaada wa hakika hauhitaji matangazo, sio lazima ugonge vichwa vya habari ndio uonekane kama msaada, kumbuka zuri chajiuza, kibaya chajitembeza.

Waswahili walinena kuwa, tenda wema nenda zako, wakaja wakaongeza kuwa, wema hauozi, lakini wema wa serikali yetu pamoja na uongozi wake ni wema wa aina gani? Ni wema huu, au uozo na unyama? Mtu mwenye akili timamu na mwenye utu ya binadamu anaweza kuwakodolea macho watu wanaokufa kutokana na njaa, ilhali pesa zinazostahili kuwasaidia, anajilimbikizia na kujiendelezea utajiri? Si huu ndio uhayawani aliyoimba msanii Nyashinski? Si haki kabisa!

    Image result for makali ya kiangazi afrika



LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...