Wednesday 25 April 2018

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu
Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu
Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie

Kitizama likotoka, hatua mepiga Sana
Katika vyombo tajika, kazi yako tumeona
Citizeni bila Shaka, wapambia kama hina
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Sauti yako nyororo, Kama chatu navutiwa
Katika giza totoro, niondowe Kama njiwa
Wanionao kiporo, Washtuke kipakuliwa
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Taka huo ujasiri, taka huo ubunifu
Kwenye kamera si siri, kazi ngumu ya kusifu
Nataka kuwa mahiri, Kama wewe mkufuu
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Tafurahi kitimiza, ndoto yangu aushini
Ninaapa kutocheza, funzo lako tathamini
Niinue Kama pweza, nyayo zako natamani
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Lulu jina Kama ua, nipambie ari yangu
Hasani mama tambua, taka uwe ngao yangu
Maza Aziza najua, kazi zako hizi tangu
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.

Natumai mesikia, ombi langu la moyoni
Siriyo natamania, ila bado ni taabani
Kama vile abiria,  lako gari niko ndani
Mwanahabari shupavu, Siri yako fichulie.
Lulu Hassan.

TATU MWAKA TUMEFIKA

Kikumbuka likotoka, mie chozi lanilenga
Japo mimba lipachika, kulikuza kajitenga
Muda bado, alimaka, tulitoe aliunga
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Kwangu likuwa zawadi, kwa dhati lisubiria
Japo shida ilizidi, Kwa Mola liangazia,
Uzazi kwangu libidi, Hata shule kuachia
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Ni mbali kifikiria, tumetoka na mwanangu
Hata njaa kilalia, kwa kuzongwa na machungu
Ma' mkwe kasaidia, pokea shukrani zangu
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Mwana ukizidi kua, mema mengi zingatia
Heshima kwako tambua, kote kote angazia
Wako baba keshajua, ndiwe wake malkia
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Japo baba nami mama, kisogo lishapeana
Kwako mwana tulisema, takulea kwa kufana
Hakikisho la kusoma, tatimiza na kwa sana
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

Sasa natia kikomo, tamati ya simulizi
Mwana menipa kisomo, cha maisha wazi wazi
Tatu mwaka siwe shimo, mengi mema na yazidi
Asante kwa Maulana, tatu mwaka tumefika.

LULU HASSAN

Siulize Ni kwa Nini, Nam enzi huyu Lulu Ueledi wake Shani, taka iga nifaulu Kwenye lugha namba wani, uliza hadi ikulu Mwanahabari shupavu...